Bukobawadau

Mushemba Foundation Yagusa Maisha ya Wengi Yatoa Misaada Kuelekea Krismasi

Taasisi ya Shirika la Mushemba Foundation, lenye makao yake makuu mkoani Kagera, limeendelea kuwa msaada wa matumaini kwa watu wasiojiweza, likiwafikia kutoka tabaka mbalimbali kwa kugawa misaada muhimu.
Mpango wa mwaka huu, uliozinduliwa rasmi tarehe 7 Desemba 2024, umeongozwa na mwanzilishi wa shirika hilo, Diakoni Josephat Mushemba.

“Kusaidia watu wasio na uwezo si jukumu la matajiri peke yao, bali ni jukumu la kila mmoja wetu,” alisema Diakoni Mushemba wakati wa hafla ya uzinduzi. “Hatuwezi kungoja tuwe na mengi ili tuguse maisha ya wengine. Upendo na huruma ndizo zawadi bora kabisa tunazoweza kuwapa wenye uhitaji.”

 
Matukio katika picha Wakati Utaratibu wa kuwafikia Msaada Wahitaji Ukiendelea
Shirika hilo limepanga kugusa kaya 170, zenye watu kati ya watatu hadi sita kila moja, kwa kugawa misaada ya vyakula, mablanketi, na vifaa vya shule. Katika hatua za kwanza za mpango huu, Diakoni Mushemba alitembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na wagonjwa na watu wenye ulemavu wa muda mrefu.

“Moyo wangu unaguswa sana ninapoona hata msaada mdogo unaweza kubadili maisha ya mtu. Huu ni wito wetu kama binadamu,” aliongeza.

Akizungumzia dhamira ya mpango huo, alisema: “Tunapoelekea Krismasi, ni wakati mwafaka wa kutafakari na kuonyesha upendo wa kweli. Hakuna baraka kubwa kuliko kuwa sehemu ya furaha ya wengine.”

Mpango huu wa kila mwaka utaendelea hadi tarehe 20 Desemba 2024, ukilenga kuwasaidia zaidi walio na uhitaji katika kipindi hiki muhimu cha sikukuu.

Shirika la Mushemba Foundation lilianzishwa mwaka 2007 kwa heshima ya Hayati Baba Askofu Dr. Samson Mushemba, likiwa na lengo la kuendeleza utume wake wa kuleta matumaini kwa yatima, wajane, wazee, na jamii kwa ujumla.

 “Hili ni jukumu ambalo hayati Baba Askofu Samson Mushemba alililiona kuwa muhimu sana. Ni heshima kubwa kuendelea na kazi hii kwa niaba yake,” alisema Diakoni Mushemba.

Kwa miaka yote, shirika hili limekuwa mwangaza wa matumaini kwa maelfu ya watu mkoani Kagera, likiendeshwa kwa maono, upendo, na juhudi za kusaidia kila mmoja bila kujali hali yake.

Mkurugenzi wa Mushemba Foundation  Joseph Mushemba pichani akiwajibika katekeleza matendo ya huruma kwa wahitaji kuelekea siku kuu ya krismasi na Mwaka Mpya

#mushemba #mushembafoundation #thanksgiving2024  #Kagera #Bukoba  #BukobawadauMatukio #IjukaOmuka #bukobawadau #bukobawadauLive


Previous Post
Bukobawadau